8 Julai 2015 - 20:51
Muda wa mazungumzo ya Iran warefushwa mpaka Ijumaa

Hapo awali Marekani na washirika wake walikuwa wakipinga haki ya Iran ya kurutubisha madini ya uranium na nyuklia lakini misimamo ya Jamhuri ya kiislamu ya Iran imefanikiwa kuifahamisha dunia kuwa haina nia ya kutengeneza kombora wala silaha za maangamizi bali inatumia teknolojia hiyo kwa matumizi ya amani ya kimaendeleo.

Shirika la habari la ABNA linalipoti kuwa: Muda wa mwisho wa kufikiwa makubaliano ya mazungumzo ya mpango wa nyuklia wa Iran yanayoendelea mjini Vienna, baina ya Iran pamoja na nchi zenye nguvu duniani umesogezwa mbele hadi Ijumaa ya wiki hii.

Taarifa ya kurefushwa mazungumzo hayo ilitolewa na Marekani licha ya kuwa leo ndio siku ya mwisho iliyopangwa makubaliano kamili kufikiwa.

Msemaji mkuu wa ujumbe wa Marekani Marie Harf amesema mazungumzo hayo yamepiga hatua lakini pia ni mazungumzo yenye uzito mkubwa kwa pande zote mbili. Ameongeza kuwa wanajali zaidi ubora wa mpango wa makubaliano kuliko muda watakaochukua kufikia makubaliano hayo ya kihistoria.

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini amesema atabaki katika mazungumzo hayo kwa siku kadhaa zijazo pamoja na pande zote husika ili kuhakikisha kuwa makubaliano yanafikiwa.

Federica Mogerini  alisema kuwa: "Tutaendelea na mazungumzo kwa siku kadhaa zijazo. Hii haimanishi kuwa tunarefusha muda wa mwisho wa kufikiwa makubaliano ya kudumu. Makubaliano ya kudumu yana uwezekano wa kupatikana ingawa sasa tunakabiliana na kipindi kigumu cha maamuzi."

Naye waziri wa nchi za nje wa urusi Sergei Lavrov amesema kuiondolea Iran vikwazo vya silaha ilivyoekewa ndio tatizo kikubwa zaidi katika mazungumzo hayo kuweza kufikiwa makubaliano, huku Iran kwa upande wake ikitaka vikwazo hivyo viondolewe vyote kwa wakati mmoja mara tu baada ya kufikia makubaliano hayo.

Hata hivyo ripoti iliyotolewa na Marekani baada ya mkutano uliopita mwezi Aprili baina ya pande hizo mbili, imesema vikwazo hivyo vitabaki kuwepo hadi mkataba wa mwisho utakapofikiwa.

Wasiwasi wa nchi za magharibi kuhusu Iran

Maafisa wa nchi za magharibi wanawasiwasi kuiruhusu Iran kununua silaha kutoka nje kutachochea mzozo unaoendelea mashariki ya kati. Iran hata hivyo pia inamchango wa pekee katika kupambana na wanamgambo wa kundi la kigaidi la Daesh nchini Iraq na Syria.

Mazungumzo hayo yanayoendelea ya mpango wa nyuklia baina ya Iran na nchi sita - Uingereza, China, Ufaransa, Ujerumani, Urusi na Marekani yanalenga kupunguza kasi mpango wa Iran wa nishati ya nyuklia kwa zaidi ya muongo mmoja ujao, na badala yake Iran itaondolewa vikwazo ilivyowekewa ambavyo vimeuathiri usafirishaji wa mafuta wa nchi hiyo pamoja na uchumi mzima kwa jumla.

Hii ni mara ya tano tangu mwaka 2013 kwa pande hizo mbili kushindwa kufikia makubaliano kamili katika muda uliopangwa. Katika mazungumzo ya hivi karibuni siku ya mwisho ya kufikiwa makubaliano ilikuwa ni Juni 30, muda ambao ulisogezwa mbele hadi leo Julai 7, na sasa umepelekwa tena mbele hadi Ijumaa ijayo, Julai 10.

Hapo awali Marekani na washirika wake walikuwa wakipinga haki ya Iran ya kurutubisha madini ya uranium na nyuklia lakini misimamo ya Jamhuri ya kiislamu ya Iran imefanikiwa kuifahamisha dunia kuwa haina nia ya kutengeneza kombora wala silaha za maangamizi bali inatumia teknolojia hiyo kwa matumizi ya amani ya kimaendeleo.

Mwisho wa habari/ 291